search

Buriani Prof. Ken Walibora Waliaula

Reading Time: 4 minutes

Ken Walibora. Mwalimu mtajika. Mwandishi wa kupigiwa mfano, mwanahabari shupavu na mtetezi wa lugha teule ya Kiswahili.

Wengi tunamkumbuka Profesa Ken kama mwandishi maarufu ambaye kazi zake ziliweza kuteka nyoyo za wapenzi wengi wa fasihi na hasa fasihi ya Kiswahili. Shuleni na vyuo mbalimbali wanafunzi wengi walitangamana na baadhi ya kazi alizoandika, kuhakiki na kuhariri, nyingine ambazo zilifundishwa katika shule za upili na kutahiniwa katika mitihani ya kitaifa ya shule za upili nchini Kenya. Kupitia uandishi wake, mitazamo ya jamii zetu juu ya masuala ya kijamii, kidini, kisiasa na kiuchumi ilisawiliwa vilivyo katika nyingi za kazi za Walibora.

Kwangu, namkumbuka na kumsherehekea Ken kwa ukwasi wake katika taaluma ya uandishi. Nyingi ya kazi za fasihi alizotoa Walibora zilifanikiwa pakubwa kuipa jamii nafasi ya kujitazama kwa lengo kuu la kujirekebisha, kujirudi, kujiboresha na kujielimisha kwa manufaa yayo na vizazi vijavyo. Na hili ndilo jukumu kuu la fasihi. Matumizi ya lugha na mbinu za uandishi havikuweza tu kuuleta mnato wa wasomaji bali pia kuwaburudisha na kuwapa wasomaji hamu ya kutangamana na kazi za fasihi na kupelekea wengi kuuenzi umaridadi na utamu wa lugha na fasihi ya Kiswahili.

Katika hadithi yake fupi Nizikeni “Papa Hapa” kwenye diwani ya Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine, Ken Walibora anamjenga mhusika Otii kuwakilisha vijana hasa wachezaji ambao huchuma riziki kutoka kwa talanta zao. Vijana hawa ambao kwa kukosa maono na maelekezo mema, hujiingiza kwenye anasa za ujana ambazo huishia kuwa na athari hasi kwa maisha yao ya baadaye. Vilevile, anauweka wazi utepetevu wa wasimamizi wa timu za michezo ambazo wachezaji wao baada ya kupatwa na matatizo (kujeruhiwa) katika harakati za kuichezea timu, hawaiwajibiki kuangazia masilahi na hali za afya zao.

Wakuu hawa huwatelekeza vijana hawa licha ya kuwa na mchango mkubwa katika mafanikio yazo.

Riwaya ya Siku Njema ambayo iliweza kushinda tuzo nyingi na iliyomweka mwangani Profesa Ken ndiyo inayopendwa na wengi. Riwaya hii iliweza kupata nafasi ya kusomwa na kutahiniwa katika mitihani ya kitaifa ya shule ya upili nchini Kenya. Katika riwaya hii, mwandishi Ken Walibora anadhamiria kuionyesha jamii kuhusu maisha ya ugumu wanayopitia watoto ambao wametengana au kutenganishwa na wazazi wao wa kuwazaa. Watoto hawa huishia kupitia machungu na mateso si haba. Kongowea Mswahili, mhusika mkuu na msimulizi wa hadithi, anakumbana na changamoto tele katika maisha yake ya utotoni. Anakosa malezi mema, upendo wa wazazi, elimu bora na anapitia wakati mgumu katika safari yake ya kujitambua. Anayoyaona akiwa na umri mdogo ni ya kuvunja moyo. Hata hivyo, anajipa moyo kwamba ipo siku ambayo itakuwa njema, siku ambayo madhila yake yatafika mwisho.

Kama mwanahabari, na kwenye juhudi zake za kibinafsi, Walibora alikuwa kwenye mstari wa mbele katika kuitetea lugha ya Kiswahili na lugha za Kiafrika. Ninamkumbuka kupitia kauli zake zilizojaa hekima hususan kuhusiana na jukumu la lugha kama chombo cha mawasiliano na sehemu ya utamaduni wetu. Kinyume na mitazamo ya baadhi, walioiona lugha yao hasa Kiswahili kuwa lugha duni na ambayo si ya kistaarabu, na kuzienzi lugha za kigeni, Ken aliwasuta sana na kuwaona kama waliojazwa na kasumba za kikoloni. Kauli ambazo wengi wa wataalam wa lugha wanaziunga mkono.

Ujio na maendeleo katika teknolojia ya habari na mawasiliano uliitishia lugha ya Kiswahili na lugha za Kiafrika hasa katika kuafiki viwango vya matumizi katika ulimwengu mpya. Hata hivyo, Ken Walibora katika kazi yake kama mwanahabari katika Sirika la Kitaifa la Utangazazi la KBC na baadaye mwanahabari na Meneja Msimamizi wa Kitengo cha Ubora wa Kiswahili katika Shirika la Habari la Nation, aliushikilia usukani barabara kuhakikisha kuwa Kiswahili kilipewa nafasi kubwa na ubora wake kudumishwa.

Jinsi alivyotangamana, kuwalea, kuwafunza na kuwaelekeza wanahabari wenza na wanafunzi wake bila shaka ni thibitisho kuwa aliipenda na kuienzi lugha hii na taaluma ya uanahabari kama nyenzo muhimu katika maendeleo ya nchi na jamii pana.

Nilitamani sana kukutana naye, kuzungumza na kupata nakala iliyotiwa sahihi ya Kitabu chake Siku Njema. Nilitamani sana kumpongeza kwa mchango wake katika ukuaji wa Kiswahili. Nilitamani sana kutangamana na kupata wosia wa moja kwa moja kutoka kinywani mwake. Nilitamani sana kupigwa picha naye kama kumbukumbu ya muda mrefu wa umahiri wake katika taaluma hii. Nilitamani sana kumpongeza kwa jinsi alivyoiwakilisha na kuiwasilisha lugha za Kiafrika na Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa. Alivyozitetea lugha za Afrika na kufunza Kiswahili kwenye vyuo vya ughaibuni na kuwakemea walioizidunisha lugha zetu. Nilitamani sana kuzungumza naye kuhusu mengi aliyoyaandika na uhusiano wa kazi zenyewe na maisha yake. Haya yote yatasalia tu hiyo; matamanio.

Nimesoma na kuyasikia mengi kumhusu Profesa Walibora. Mja mwenye utu, mpole kwa kusema na mwenye msimamo thabiti na nia isiyotetereka. Alivyowapenda wote na kuwaenzi. Upole wake uliwavutia wengi. Yamesemwa mengi kuhusu ukarimu na juhudi zake katika kila alichokifanya.

Kwake alitazamia siku njema, siku ambayo mambo yatakuwa kinyume na yalivyo. Kinyume na changamoto zinazoikumba jamii na watu binafsi. Siku ambayo binadamu watajawa na utu na kuwaenzi wengine na kuwa wa msaada wa kweli. Siku ambayo mapenzi yatakuwa ya kweli na yanayoleta furaha kwenye mtima. Siku ambayo matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yatakuwa yamepungua mno. Na kwangu, hii itakuwa Siku Njema.

Kwa famlia, ndugu na marafiki, kwa wapenzi wa Kiswahili, wataalam wa lugha, isimu na fasihi, wasomi, waandishi, wahariri na wachapishaji, waalimu na wanafunzi wa Kiswahili; poleni. Makiwa kwa wote ambao mauko ya bingwa wetu yamewapa majonzi na kuwaliza. Mola awafariji na kuwapa nguvu za kustahimili machungu ya kuondoka ghafla kwa ndugu yetu.

Ni bayana na kweli kwamba mti mkuu ukianguka, wana wa ndege huyumba. Safiri salama ndugu Ken, buriani.

Evans Monari Nyangaresi

Mtaalam wa Utafsiri na Usanifu Makala

Mwalimu wa Kiswahili – Shule ya Upili ya Wasichana ya Buruburu

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x